Kamati ya Bodi ya Uwekezaji na Fedha WHI Yatembelea Mradi wa Nyumba 101 Mikocheni

0
062A0062
Ads

Dar es Salaam, Tanzania — Kamati ya Bodi ya Uwekezaji na Fedha ya Watumishi Housing Investments (WHI) imefanya ziara ya ukaguzi katika eneo la Mikocheni, ambako mradi wa ujenzi wa nyumba 101 unaendelea kutekelezwa. Mradi huo, ambao ulianza rasmi mwezi Septemba 2024 baada ya kukabidhiwa kwa mkandarasi mwezi Agosti, umefikia hatua ya asilimia 20 ya utekelezaji.

Katika ziara hiyo, wajumbe wa kamati walipata fursa ya kujionea mwenendo wa mradi ambao tayari umeonesha mafanikio ya awali, ambapo nyumba zote 101 zimeuzwa kabla ya kukamilika kwa ujenzi. Mkandarasi anayesimamia kazi hiyo alieleza kuwa utekelezaji unaendelea kwa kuzingatia viwango vya ubora, na kutumia vifaa vya kisasa kuhakikisha nyumba zinajengwa kwa ubora unaostahili.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa WHI, Arch. Sephania Solomon, aliishukuru kamati kwa kutembelea mradi na kutoa maoni ya kitaalamu. Alisema kuwa WHI itaendelea kuandaa na kutekeleza miradi mipya ili kuwafikia watumishi wengi zaidi. Aidha, alihimiza watumishi wa umma kuendelea kujiunga na Mfuko wa Faida (Faida Fund) ambao umelenga kuwawezesha kiuwekezaji na kuwapa fursa ya kumiliki nyumba kwa urahisi.

Ads

Mwenyekiti wa Kamati ya Bodi ya Uwekezaji na Fedha, Bw. Celestin Muganga, alieleza kuridhika na namna mradi unavyoendelea kutekelezwa. Alisema kamati imefarijika kuona mradi ukisonga mbele kwa kasi na ubora, huku akihimiza WHI kuongeza juhudi katika kuanzisha miradi ya nyumba za bei nafuu ili kuongeza upatikanaji wa makazi kwa watumishi wa kipato cha chini na cha kati.

Watumishi Housing Investments inaendelea kuwa taasisi muhimu katika sekta ya makazi nchini, kwa kujikita katika ujenzi wa nyumba za gharama nafuu zinazolenga kuwahudumia watumishi wa umma. Mafanikio ya taasisi hiyo yameifanya kutambulika katika ngazi ya bara, ambapo ilipata tuzo ya taasisi bora barani Afrika kwa ujenzi wa nyumba nafuu.

Mradi wa nyumba 101 Mikocheni unatarajiwa kukamilika mwezi Machi 2026, na kuanza kukabidhiwa kwa wanunuzi kwa wakati huo.

Spread the love
Ads

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *