Mama Apatikana na Hatia ya Kuuza Mtoto kwa Mganga

Tukio la kusikitisha na kutisha limeutikisa moyo wa taifa la Afrika Kusini, baada ya mama mmoja kupatikana na hatia ya kumteka na kumsafirisha binti yake wa miaka sita, ambaye hadi sasa hajulikani alipo tangu kutoweka kwake zaidi ya mwaka mmoja uliopita.
Kelly Smith, mama wa mtoto huyo aliyejulikana kama Joshlin Smith, alifikishwa mahakamani pamoja na mpenzi wake, Jacquen Appollis, na rafiki yao wa karibu, Steveno van Rhyn. Watatu hao walikamatwa baada ya Joshlin kutoweka katika eneo la Saldanha Bay, karibu na mji wa Cape Town, mnamo Februari mwaka jana.
Siku ya Ijumaa, mahakama iliwapata wote watatu na hatia ya kuteka nyara na kumsafirisha mtoto huyo. Hapo awali walikana mashtaka yote, lakini ushahidi uliowasilishwa uliwafanya wakutwe na hatia.
Kesi hiyo iliendeshwa katika Kituo cha Kazi cha Saldanha (Saldanha Multipurpose Centre) na kuvuta hisia kubwa za wananchi. Mamia ya watu walifurika nje ya jengo la mahakama wakisubiri uamuzi wa Jaji Nathan Erasmus kwa hamu na hofu. Barabara za jirani zilifungwa, huku polisi wakiimarisha ulinzi ndani na nje ya eneo hilo.

Hadi sasa, licha ya juhudi kubwa za uokoaji na matangazo ya kutafutwa kwa Joshlin, bado hajapatikana. Kisa chake kimeacha maumivu kwa familia, jamii, na taifa kwa ujumla.
Katika ushahidi uliowasilishwa mwezi Machi, upande wa mashtaka ulimtuhumu Kelly kwa “kumuuza, kumsafirisha au kumbadilisha” mtoto wake na kisha kudanganya kuhusu kutoweka kwake. Ushahidi huo ulitolewa na mashahidi mbalimbali, wakiwemo watu waliokuwa jirani na familia hiyo.
Shahidi muhimu aliyetikisa mahakama alikuwa Lourentia Lombaard, jirani na rafiki wa karibu wa Kelly, ambaye aliamua kuwa shahidi wa serikali. Lombaard alisimulia mbele ya mahakama jinsi Kelly alivyomwambia kuwa alifanya “kitendo cha kijinga” kwa kumuuza Joshlin kwa mganga wa kienyeji (sangoma), ambaye alidaiwa kuwa na nia ya kumchukua mtoto huyo kwa sababu ya macho na ngozi yake.
Kwa upande mwingine, mchungaji wa eneo hilo alitoa ushahidi kwamba aliwahi kumsikia Kelly akizungumza kuhusu kuuza watoto wake kwa kiasi cha randi 20,000 kwa kila mtoto (takribani dola 1,100 za Kimarekani), huku akiongeza kuwa alikuwa tayari hata kuwauza kwa bei ya chini ya dola 275.
Tukio hili limeacha maswali mengi kwa jamii ya Afrika Kusini: je, Joshlin bado yuko hai? Yuko wapi? Na je, kuna watu wengine nyuma ya pazia waliohusika katika biashara hii ya kikatili?
Mpaka sasa, familia na wananchi wanaendelea kuomba haki kamili ipatikane, na muhimu zaidi, Joshlin apatikane salama.