Serikali Kushirikiana na Waandaaji wa Tuzo za Muziki wa Injili Afrika Mashariki

0
image
Ads

Serikali imeonyesha nia ya kushirikiana na waandaaji wa Tuzo za Muziki wa Injili Afrika Mashariki (East Africa Gospel Awards – EAGMA) kwa lengo la kuinua vipaji vya wanamuziki wa nyimbo za injili na kuhakikisha wanapata nafasi zaidi za kutangaza kazi zao.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi wa tuzo hizo, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Sanaa kutoka Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Emmanuel Ishengoma, alieleza kuwa tuzo hizi ni hatua muhimu katika historia ya muziki wa injili, kwani zinafanyika kwa mara ya kwanza.

Amebainisha kuwa ni lazima kuhakikisha tuzo hizi zinakuwa endelevu na kuwa na mpango madhubuti wa muda mrefu ili ziwe na manufaa kwa kizazi cha sasa na kijacho.

Ads

“Muziki wa injili una nafasi kubwa katika jamii yetu, kwani unapowaimbia watu ujumbe wa kiroho, unasaidia pia katika kujenga maadili mema. Hivyo basi, serikali iko tayari kushirikiana nanyi ili kuhakikisha tunaleta mabadiliko chanya katika tasnia hii,” alisema Dkt. Ishengoma.

Ameongeza kuwa wazo hili linapaswa kupanuka zaidi na kutazama upeo mpana wa bara zima la Afrika badala ya kuishia katika nchi za Afrika Mashariki pekee.

Kwa upande wake, Rais wa Shirikisho la Muziki Tanzania na Mwenyekiti wa Chama cha Muziki Tanzania, Ado November, alisema kuwa ushirikiano wa Tanzania na EAGMA umefanikisha kuhusisha mataifa mbalimbali ikiwemo Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, na Sudani Kusini.

Amesema kuwa tuzo hizi zitakuwa chachu ya maendeleo kwa wanamuziki wa injili, kwani kwa muda mrefu wamekuwa wakihangaika kukuza vipaji vyao bila mfumo rasmi wa kutambua juhudi zao.

“Tuzo hizi ni mwanzo mpya kwa wasanii wa muziki wa injili, kwani zitawapa motisha na kuthibitisha kuwa kazi zao zinathaminiwa. Pia, zitachangia kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwao,” alisema Ado November.

Naye Muandaaji Mkuu wa Tuzo za EAGMA, Magreth Chacha, alifafanua kuwa mpango huu unalenga kuwaleta pamoja wasanii wa injili, wadau wa muziki, na mashabiki kutoka nchi mbalimbali za Afrika Mashariki.

Amesema lengo kubwa ni kutumia muziki wa injili kama nyenzo ya kuleta mabadiliko katika jamii, hasa kwa vijana ambao mara nyingi hukumbwa na vishawishi vya kuimba muziki wa kidunia.

“Tunaamini kuwa kupitia tuzo hizi, tutaweza kuvutia vipaji vingi zaidi na kuwatia moyo wale waliokuwa wakisita kujitokeza. Hili ni jukwaa la kutambua mchango wa muziki wa injili katika kuhamasisha jamii na kuleta faraja kwa watu wengi,” alisema Chacha.

Kwa mujibu wa waandaaji, tuzo hizo pia zinalenga kuendeleza muziki wa injili hadi katika jukwaa la kimataifa na kuwapa wasanii wa Afrika Mashariki nafasi ya kuonyesha vipaji vyao kwa hadhira kubwa zaidi.

Spread the love
Ads

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *