Virusi Hatari Vinavyotokana na Panya

Hantavirus ni ugonjwa adimu lakini hatari unaosababishwa na virusi vinavyotokana na panya. Hivi karibuni, ugonjwa huu umechukua maisha ya Betsy Arakawa, mke wa mshindi wa tuzo ya Oscar Gene Hackman, baada ya kupata matatizo makubwa ya kupumua yanayohusiana na Hantavirus Pulmonary Syndrome (HPS).
Hantavirus ni Nini na Unasambaa Vipi?
Hantavirus ni mkusanyiko wa virusi vinavyopatikana kwa panya na kusambaa kwa binadamu kupitia:
- Kuvuta hewa iliyo na chembechembe za kinyesi, mkojo, au mate ya panya.
- Kugwaruzwa au kung’atwa na panya.

Kwa mujibu wa Kituo cha Kudhibiti na Kuzuia Magonjwa (CDC), virusi hivi husababisha magonjwa mawili makubwa:
1. Hantavirus Pulmonary Syndrome (HPS)
Huu ni ugonjwa wa mapafu unaoathiri zaidi Amerika Kaskazini. Dalili zake za awali zinafanana na mafua, ikiwa ni pamoja na:
- Homa kali
- Uchovu na maumivu ya misuli
- Kichwa kuuma
- Matatizo ya tumbo kama kichefuchefu na kutapika
Baada ya siku chache, ugonjwa huu unaweza kugeuka na kusababisha matatizo makubwa ya kupumua, hatimaye kupelekea kifo.
2. Hemorrhagic Fever with Renal Syndrome (HFRS)

Aina hii ya ugonjwa huathiri zaidi figo na inaweza kusababisha kutokwa na damu ndani ya mwili. HFRS inapatikana zaidi barani Ulaya na Asia.
Je, Kuna Tiba ya Hantavirus?
Kwa sasa, hakuna tiba maalum ya ugonjwa huu. Wagonjwa wenye dalili kali hulazwa hospitalini na kupewa matibabu ya kupunguza athari za ugonjwa huo.
Jinsi ya Kujikinga na Hantavirus
Kwa kuwa Hantavirus unasambazwa na panya, njia bora ya kujikinga ni kuhakikisha unadhibiti uwepo wa panya katika mazingira yako. Hii ni pamoja na:
- Kuzuia upatikanaji wa chakula na makazi kwa panya kwa kudumisha usafi.
- Kutumia barakoa na glovu unapofanya usafi wa kinyesi cha panya.
- Kutumia maji na dawa maalum kusafisha maeneo yanayoweza kuwa na kinyesi cha panya badala ya kufagia au kutumia upepo.
Hantavirus ni ugonjwa unaoweza kuzuiwa ikiwa tahadhari sahihi zitachukuliwa. Ni muhimu kuwa na ufahamu wa hatari zake ili kulinda afya yako na ya jamii inayokuzunguka
SOMA HII: Mambo 5 usiyoyajua kuhusiana na Jumatano ya majivu