VODACOM NA ZICTIA WASHIRIKIANA KUBORESHA MAWASILIANO ZANZIBAR

Katika hatua muhimu ya kuimarisha mawasiliano na kuchochea maendeleo ya kidijitali Zanzibar, Vodacom Tanzania PLC imesaini makubaliano ya kimkakati na Shirika la Miundombinu ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano Zanzibar (ZICTIA). Ushirikiano huu unalenga kuboresha huduma za mawasiliano kwa kutumia miundombinu ya nyaya za chini ya bahari inayomilikiwa na serikali ya Zanzibar.
Makubaliano haya yalisainiwa katika ofisi za Wizara ya Ujenzi, Mawasiliano, na Uchukuzi Zanzibar mnamo Februari 26, 2025, huku hafla hiyo ikihudhuriwa na viongozi mbalimbali, akiwemo Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dkt. Khalid Salum Mohamed.
Serikali Yapongeza Jitihada za Vodacom

Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Dkt. Khalid Salum Mohamed aliipongeza Vodacom Tanzania kwa juhudi zake za kuimarisha mawasiliano Zanzibar. “Tunaishukuru Vodacom kwa kuendelea kuwekeza katika minara ya mawasiliano, hatua ambayo imeongeza kasi ya intaneti na upatikanaji wa huduma za kidijitali kwa wananchi wetu. Ushirikiano huu utasaidia kuimarisha huduma za serikali mtandao, elimu mtandao, afya mtandao, na biashara mtandao.”
Aliongeza kuwa serikali inaendelea kuweka mazingira wezeshi kwa kampuni za mawasiliano ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za intaneti kwa gharama nafuu.
Vodacom Yajidhatiti Kuimarisha Mawasiliano
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Mtandao wa Vodacom Tanzania, Andrew Lupembe, aliyemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom, alisema, “Lengo letu ni kuhakikisha kuwa Zanzibar inakuwa na mawasiliano ya kisasa na yenye kasi ya juu. Kwa kushirikiana na ZICTIA, tunahakikisha kuwa wananchi, wafanyabiashara, na taasisi wanapata huduma bora za mawasiliano bila changamoto.”
Lupembe aliongeza kuwa Vodacom itaendelea kushirikiana na serikali na wadau wengine katika kuboresha miundombinu ya mawasiliano na kuleta suluhisho za kidijitali zinazochochea ukuaji wa uchumi wa visiwa hivyo.
ZICTIA Yasisitiza Umuhimu wa Ushirikiano

Mkurugenzi Mkuu wa ZICTIA, Mhandisi Shukuru Awadh Suleiman, alieleza kuwa ushirikiano huu utasaidia kufanikisha malengo ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya TEHAMA. “Miundombinu ya nyaya za chini ya bahari ni rasilimali muhimu kwa maendeleo ya kidijitali. Tuna furaha kuona Vodacom ikitumia rasilimali hii ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za intaneti na mawasiliano.”

Hatua Hii Yaleta Mustakabali Mpya wa Kidijitali Zanzibar
Kwa mujibu wa makubaliano haya, Zanzibar itanufaika na mtandao wa kasi ya juu, ambao utaimarisha shughuli za kibiashara, elimu, na huduma za serikali. Ushirikiano kati ya Vodacom na ZICTIA unaweka msingi mzuri wa maendeleo ya kidijitali visiwani humo, na kuhakikisha kuwa Zanzibar inakuwa kitovu cha TEHAMA katika ukanda wa Afrika Mashariki.