WHI Yamuaga Rasmi Dkt. Fred Msemwa

Watumishi Housing Investment (WHI) imefanya hafla maalum kumuaga aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wake, Dkt. Fred Msemwa, kufuatia uteuzi wake na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kuwa Katibu Mtendaji wa Tume ya Mipango ya Taifa.

Hafla hiyo, iliyofanyika katika makao makuu ya WHI jijini Dar es Salaam, ilihudhuriwa na wafanyakazi wa taasisi hiyo.
Katika hotuba yake ya kuaga, Dkt. Msemwa alitoa shukrani kwa WHI kwa ushirikiano alioupata katika kipindi cha uongozi wake na kuhimiza mshikamano, ubunifu, na uendelezaji wa miradi yenye tija kwa Watanzania. “WHI imepiga hatua kubwa katika kutoa makazi bora na nafuu. Nawaomba muendelee kushirikiana kwa uaminifu ili kuhakikisha taasisi inasonga mbele zaidi,” alisema.

WHI imejipambanua kama taasisi inayoongoza katika ujenzi wa nyumba za gharama nafuu nchini Tanzania. Kwa miaka kadhaa, imefanikiwa kujenga maelfu ya nyumba kwa ajili ya makundi mbalimbali, hasa wale wa kipato cha chini na cha kati. Kupitia miradi yake, taasisi hii imewezesha Watanzania wengi kumiliki makazi bora kwa gharama nafuu huku ikiimarisha ushirikiano na sekta za kifedha kwa ajili ya upatikanaji wa mikopo nafuu ya nyumba.





Moja ya mafanikio makubwa ya WHI ni kuanzisha Mfuko wa Faida Fund, ambao unalenga kusaidia wananchi kumiliki nyumba kwa njia rahisi zaidi kupitia mifumo ya kifedha jumuishi. Mpango huu umeleta mabadiliko makubwa katika sekta ya makazi kwa kutoa fursa za umiliki wa nyumba kwa Watanzania wengi zaidi.
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa WHI, Arch. Solomon, alimshukuru Dkt. Msemwa kwa mchango wake mkubwa na kuahidi kuendeleza miradi iliyoanzishwa chini ya uongozi wake. “WHI itaendelea kujikita katika kutoa suluhisho bunifu kwa Watanzania kwa kuhakikisha tunajenga nyumba bora na za gharama nafuu. Tunaahidi kuendeleza jitihada zote alizoanzisha Dkt. Msemwa kwa manufaa ya Taifa,” alisema Arch. Solomon.
Katika hafla hiyo, wafanyakazi wa WHI walimpatia zawadi mbalimbali kama ishara ya heshima na shukrani kwa mchango wake ndani ya taasisi hiyo. Wafanyakazi walieleza kuwa uongozi wake umeacha alama isiyofutika, na walimtakia mafanikio mema katika majukumu yake mapya ndani ya Tume ya Taifa ya Mipango.
WHI inaendelea kujizatiti kuhakikisha Watanzania wengi zaidi wanapata makazi bora na nafuu, sambamba na kuimarisha nafasi yake kama taasisi inayoongoza katika sekta ya maendeleo ya makazi nchini Tanzania.

SOMA HII: Dunia Kwenye Hatari Mpya ya HIV Baada ya Msaada Kusitishwa