Washindani Wakuu wa Dr. Janabi Ukurugenzi WHO Afrika

Mbio za nafasi ya Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika wa Shirika la Afya Duniani (WHO) zimezidi kuwa ngumu, huku wagombea watano wakijitokeza kutafuta nafasi hiyo muhimu. Uchaguzi wa mkurugenzi huyo unatarajiwa kufanyika Mei 18, 2025, na utaamua ni nani atakayechukua jukumu la kuongoza juhudi za WHO kukabiliana na changamoto kubwa za afya barani Afrika. Katika kinyang’anyiro hiki, Profesa Mohamed Janabi, mtaalamu maarufu wa afya kutoka Tanzania, anapigania nafasi hiyo, akiwa na mafanikio makubwa na changamoto za kipekee.
Prof. Mohamed Janabi (Tanzania)
Prof. Janabi, ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH), ni mgombea pekee kutoka kusini mwa Jangwa la Sahara. Ana uzoefu wa miaka mingi katika sekta ya afya, akiwa ameongoza tafiti muhimu na kutoa michango ya kipekee katika afya ya umma. Pia ni Mhadhiri katika Chuo Kikuu cha Muhimbili na ameendelea kuwa mshauri wa Rais Samia Suluhu Hassan kuhusu masuala ya afya.

Hata hivyo, Prof. Janabi anakutana na upinzani mkali kutoka kwa wagombea wanne kutoka Afrika Magharibi, ambao pia wanahusishwa na michango makubwa katika sekta ya afya. Hawa ni Moustafa Mijiyawa kutoka Togo, Dk. Boureima Hama Sambo kutoka Niger, Dk. N’Da Konan Michel Yao kutoka Ivory Coast, na Mohamed Lamine Dramé kutoka Guinea. Kila mmoja wao anayejiandaa kwa kinyang’anyiro hiki, ana historia ya kipekee na michango muhimu katika afya ya umma na ushirikiano wa kimataifa.
Moustafa Mijiyawa-Togo

Moustafa Mijiyawa, ambaye alikuwa Waziri wa Afya wa Togo kuanzia 2015 hadi 2024, anajivunia uzoefu wa miaka zaidi ya 30 katika tiba ya magonjwa ya baridi yabisi. Dkt. Mijiyawa pia aliongoza Shule ya Kitaifa ya Wasaidizi wa Matibabu nchini Togo na ni mtaalamu wa rheumatology.
Dk Boureima Hama Sambo (Niger)

Dkt. Boureima Hama Sambo kutoka Niger, kwa upande mwingine, anajivunia uzoefu wa zaidi ya miaka 30 katika sekta ya afya, akiwa ametumika kama Mwakilishi wa WHO katika nchi mbalimbali, ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Alikuwa pia mmoja wa wagombea katika mchakato wa uchaguzi wa mwaka jana, lakini alishindwa na Dk. Faustine Ndugulile wa Tanzania.
Dk. N’Da Konan Michel Yao, Ivory Coast

Dkt. N’Da Konan Michel Yao kutoka Ivory Coast ni mtaalamu wa afya ya umma na mtafiti mashuhuri, ambaye amechapisha tafiti nyingi kuhusu magonjwa ya kuambukiza barani Afrika. Alikuwa miongoni mwa wagombea wa mwaka jana na alishindwa na Ndugulile.
Mohamed Lamine Dramé, Guinea

Mohamed Lamine Dramé kutoka Guinea anajivunia uzoefu mkubwa wa kimataifa katika afya ya umma, akiwa ametumikia kwa miaka zaidi ya 20 kama mtaalamu wa afya katika mashirika mbalimbali ya kimataifa, ikiwa ni pamoja na WHO. Pia ana historia ya kutoa ushauri wa afya kwa nchi za Kiafrika na mashirika ya kimataifa.
Kwa sasa, ugumu wa uchaguzi huu unazidi kutawala, na kila mmoja wa wagombea anatumai kuwa atashinda nafasi hii muhimu, ambayo itakuwa na athari kubwa kwa afya ya umma barani Afrika. Wakati huu wa uteuzi, ni wazi kuwa historia ya kila mgombea itakuwa na uzito mkubwa katika kuamua ni nani atakayechukua uongozi wa Kanda ya Afrika wa WHO.
SOMA HII: Dunia Kwenye Hatari Mpya ya HIV Baada ya Msaada Kusitishwa