UGONJWA WA MPOX ULIVYOGUNDULIKA TANZANIA

Tanzania imethibitisha kesi mbili za ugonjwa wa Mpox baada ya uchunguzi wa maabara kuthibitisha uwepo wa virusi hivyo kwa wahisiwa wawili. Waziri wa Afya, Mhe. Jenista Mhagama, ametangaza taarifa hiyo leo, Machi 10, 2025, akieleza hali ya ugonjwa huo nchini.
Kwa mujibu wa Waziri Mhagama, Wizara ya Afya ilipokea taarifa za wahisiwa mnamo Machi 7, 2025, kupitia mifumo yake ya ufuatiliaji wa magonjwa. Wahisiwa hao walikuwa na dalili kama vipele vilivyojitokeza usoni, mikononi, miguuni, na sehemu nyingine za mwili. Aidha, mmoja wa wahisiwa ni dereva wa gari la mizigo aliyesafiri kutoka nchi jirani hadi Dar es Salaam.
Baada ya kuchukua sampuli na kuzipeleka Maabara ya Taifa kwa uchunguzi, majibu yaliyotolewa Machi 9, 2025, yalithibitisha kuwa wahisiwa hao wawili wameambukizwa virusi vya Mpox.
Hatua Zinazochukuliwa na Serikali

Wizara ya Afya, kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI na vituo vya kutolea huduma za afya, inaendelea na ufuatiliaji wa ugonjwa huu ili kubaini wahisiwa wengine na kuwapatia huduma stahiki. Serikali pia inaimarisha juhudi za kudhibiti maambukizi kwa:
✅ Ufuatiliaji wa magonjwa katika ngazi zote
✅ Upimaji wa wasafiri wanaoingia na kutoka nchini
✅ Kuongeza elimu ya afya kwa umma kuhusu kujikinga na maambukizi
Chanzo cha Maambukizi na Njia za Kujikinga
Mpox husababishwa na virusi vinavyopatikana kwa wanyama wa jamii ya nyani, na binadamu anaweza kupata maambukizi kwa kugusana na wanyama hao, majimaji yao, au kula nyama iliyoambukizwa. Ugonjwa huu pia huweza kuambukizwa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine kupitia mgusano wa moja kwa moja.
Wananchi wanahimizwa kuchukua tahadhari kwa kuepuka kugusana na wagonjwa, kudumisha usafi wa mikono, na kuripoti dalili zozote zinazohusiana na ugonjwa huu katika vituo vya afya vilivyo karibu.
Kwa taarifa zaidi kuhusu ugonjwa wa Mpox na jinsi ya kujikinga, endelea kufuatilia matangazo rasmi kutoka Wizara ya Afya.
SOMA HII: Virusi Hatari Vinavyotokana na Panya